MARA baada ya kikosi cha Simba kutua nchini, haraka Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mhispania, Pablo Franco alifanya kikao kizito na wachezaji wake wote kambini akiwemo Mkongomani, Hennock Inonga katika kuelekea Kariakoo Dabi.
Dabi hiyo inatarajiwa kuzikutanisha timu kongwe za Simba dhidi ya Yanga, mchezo ambao utapigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo tishio kubwa hadi sasa kwa mabeki wa Simba ni uwezo mkubwa wa kutupia mabao anaouonyesha Fiston Mayele ambaye amefunga mabao 12 kwenye ligi kuu.
Kikosi cha Simba kilirejea nchini usiku wa Jumatatu kikitokea Afrika Kusini walipokwenda kucheza mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Simba waliondolewa na Orlando Pirates kwa penalti 4-3.
Mmoja wa mabosi wa benchi la ufundi la timu hiyo, amesema kuwa kocha huyo katika kikao hicho kikubwa aliwataka kusahau matokeo ya mchezo uliopita dhidi ya Pirates na badala yake kuelekeza nguvu katika dabi.
Bosi huyo alisema baadhi ya wachezaji wake wanahitaji kutengenezwa kisaikolojia akiwemo Inonga ambaye alionekana kuumia mara baada ya kukosa penalti katika mchezo dhidi ya Pirates.
Aliongeza kuwa kocha huyo amewataka wachezaji wake kuelekeza nguvu katika dabi na kikubwa kupata pointi tatu zitakazowafariji mashabiki wao wanaowasapoti kila siku.
“Kocha hivi sasa anatengeneza saikolojia ya wachezaji baada ya mchezo dhidi ya Pirates ambao tulifungwa kwa penalti na kuondolewa katika shirikisho.
“Anaamini kuwa baadhi ya wachezaji wameumizwa baada ya matokeo hayo mabaya, kwani yameharibu malengo yetu ambayo ni kufika nusu fainali shirikisho,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa: “Kila baada ya mchezo kunakuwepo na kikao cha wachezaji na benchi la ufundi na kikubwa kupeana moyo na kukumbushana majukumu.
“Hivyo kocha alifanya kikao na wachezaji wake wote mara baada ya mchezo dhidi ya Pirates na kikubwa aliwataka kusahau matokeo yaliyopita na badala yake nguvu na akili kuzielekeza mchezo wa dabi.”