KIPA namba moja wa Simba, Aishi Manula ambaye alikaa langoni kwenye mechi zote za kimataifa msimu huu wa 2021/22 ambazo Simba imecheza amesema kuwa wamejiskia vibaya kutolewa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho.
Mbele ya Orlando Pirates dk 90 za Uwanja wa Mkapa, Manula aliweza kushuhudia timu yake ikishinda bao 1-0 na walipowafuata kwenye ngwe ya pili nchini Afrika Kusini,Manula alishuhudia timu yake ikifungwa bao 1-0 na yeye alikaa langoni dk zote 180.
Katika changamoto ya penalti mbele ya Orlando Pirates Manula aliokoa penalti moja huku nne zote zikizama nyavuni na kwa Simba alishuhudia wapigaji wawili wakikosa penalti na kufanya wapinzani wao wasonge mbele kwa jumla ya penalti 4-3.
Air Manula amesema kuwa hawakutarajia matokeo hayo ambayo walipata ugenini.
“Tunajisikia vibaya kwa matokeo ambayo tumeyapata, tunamshukuru Mungu tumeweza kurudi salama lakini kile ambacho tumekipata hatujafurahia kwani ilikuwa ni kazi kubwa.
“Ambapo tumefika leo hatuwezi kukwepa kikubwa tunajua kwamba mechi za away , (ugenini) zinakuaje ila imekuwa hivi na kwa namna hiyo yale ya nje tuliyazoea ila ya ndani matokeo tulishindwa kupata.
“Binafsi ninaona kwamba tunazidi kukua kama timu na robo fainali hii ipo tofauti kabisa na mwendelezo unakuwa mzuri kuliko msimu uliopita,”