MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele, amesema kuwa deni kubwa alilobakiza kwa sasa ni kuifunga Simba pekee, mara baada ya kumalizana na Namungo kama ambavyo aliwaahidi mashabiki.
Mayele Jumamosi alifanikiwa kuifungia Yanga bao moja katika ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Mara baada ya kufanikiwa kuifungia Yanga bao hilo, Mayele amesema kuwa katika ahadi ambazo aliziahidi kwa mashabiki, sasa amebaki na deni moja nalo ni kufunga bao katika mchezo wao dhidi ya Simba, Jumamosi.
“Mashabiki walikuwa wakinidai kuzifunga timu mbili ambazo ni Simba na Namungo, niliweka ahadi hii kwao kwa kuhakikisha kuwa nazifunga hizi timu, nashukuru kuona nimefanikiwa kufanya hivyo dhidi ya Namungo.
“Hivyo kwa sasa nina deni katika mchezo dhidi ya Simba kuhakikisha kuwa nafunga goli (bao) kwa ajili yao, sio rahisi kwa kuwa mabeki hawatakubali kuona nafunga lakini nitapambania hilo,” amesema Mayele.
Kwenye ligi Mayele amefunga jumla ya mabao 12 na ana pasi tatu za mabao kati ya mabao 35 ambayo yamefungwa na Yanga.