KUMEKUCHA sasa leo ni Yanga v Namungo, Uwanja wa Mkapa ngoma inatarajiwa kupigwa ikiwa ni Aprili 23,2022.
Kazi kubwa ni kwa vinara Yanga wenye pointi 51 watakapokuwa wakimenyana na Namungo FC iliyo na pointi 29 ndani ya ligi.
Ugumu wao huwa unakuwa namna hii:-
Wakali wa nyavu
Kwa Yanga wao wanaye mzee wa kutetema, Fiston Mayele amaye ametupia mabao 11 na pasi tatu kati ya mabao 33 ambayo yamefungwa na timu hiyo akiwa amecheza mechi 19.
Relliats Lusajo ni namba moja kwa utupiaji Namungo akiwa ametupia mabao 10 na pasi mbili kati ya mabao 25 yaliyofungwa na timu hiyo.
Lusajo kaanza kikosi cha kwanza kwenye mechi 14 msimu huu wa 2021/22.
Wakali wa pasi za mwisho
Ni Said Ntibanzokiza huyu ni mkali wa pasi za mwisho kwa Yanga akiwa ametengeneza jumla ya pasi nne za mabao pia ni mpigaji wa mipira iliyokufa.
Aliwapa adhabu Namungo walipokutana kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, Uwanja wa Ilulu.
Kwa Namungo FC wenye pasi nyingi wanatoa pasi mbilimbili ikiwa ni pamoja na Obrey Chirwa,Hashim Manyanya na Lusajo.
Kisiki dk 450
Mechi 5 ambazo wamekutana kwenye dk 450 hakuna timu liyoweza kusepa na pointi tatu mazima zaidi ya kugawana pointi mojamoja kila timu likutana na kisiki cha mpingo kwa kushindwa kuweza kushinda.
Machi 15, 2020, Uwanja wa Majaliwa ilikuwa msimu wa kwanza kwa timu hizo kumenyana kwenye ligi na ubao ulisoma Namungo 1-1 Yanga, mzunguko wa pili Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Yanga 2-2 Namungo ilikuwa ni Juni 24,2020.
Msimu wa pili mzunguko wa kwanza ubao ulisoma Yanga 1-1 Namungo na ule mzunguko wa pili ngoma ilikuwa Namungo 0-0 Yanga.
Msimu wa tatu kukutana ilikuwa Uwanja wa Ilulu ambapo baada ya dk 90 ubao ulisoma Namungo 1-1 Yanga.
5/5
Kwenye mechi tano ambazo wamekutana ni mabao 10 yamefungwa huku kila timu ikifunga mabao matano na ni mchezo mmoja pekee uliochezwa Mei 15,2021 haukuweza kuleta bao kwenye mchezo huo.
Mchezo wao wa mzunguko wa kwanza msimu huu, Yanga waliweza kupata bao kwa mkwaju wa penalti iliyosababishwa na Feisal Salum na mtupiaji alikuwa ni Said Ntibanzokiza.
Msikie Haji Manara
Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara amesema kuwa kila mchezo ni muhimu kupata ushindi na wanawaheshimu wapinzani wao.
“Tunajua kwamba mchezo wetu ujao dhidi ya Namungo utakuwa mgumu na ushindani mkubwa lakini tunahitaji kushinda,tunawaheshimu wapinzani hilo lipo wazi lakini wachezaji wanajua malengo yetu ni kutwaa ubingwa,”.
Huyu hapa Kihwelo
Jamhuri Kihwelo, kocha msaidizi wa Namungo FC,amesema kuwa pongezi kubwa kwa wachezaji kwa namna wanavyofanya na Imani ni kupata matokeo mechi zijazo.
“Ushindi wa mabao 3-1 Uwanja wa Ilulu inatupa ari na morali wa kufanya vizuri, tunajua kwamba mchezo wetu ujao ni dhidi ya Yanga tunaamini kwamba tutafanya vizuri na malengo yetu yataweza kutimia,”.