SIMBA WAAMUA KUKODI ULINZI AFRIKA KUSINI

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kwamba umeamua kufanya jambo la kitofauti kwa kukodi gari la ulinzi kwenye misafara yao wanapokuwa nchini Afrika Kusini baada ya wageni wao Orlando Pirates kugoma kuwapa huduma hiyo.

Jana Aprili 22, wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa ambao ni Simba waliweza kuwasili nchini Afrika Kusini kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao dhidi ya Orlando Pirates unaotarajiwa kuchezwa kesho Aprili 24.

Barbara Gonzalez, Mtendaji Mkuu wa Simba amesema kuwa wanatambua kwamba wanahitaji ulinzi na kwa kuwa hawakupewa (Escort) imewalazimu waweze kukodi ulinzi kwa kushirikiana na Balozi wa Tanzania.

“Kwa sasa hali imekuwa tofauti na awali tumekosa na tulichokifanya baada ya kuona hatujapewa ulinzi tumeamua kuwekeza nguvu kwenye ulinzi na kwa kushirkiana na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini tumeweza kukodi ulinzi.

“Kikubwa tunataka kuona kwamba tunaweza kusonga mbele na tunajua kwama tukipata sare ama kushinda tunasonga mbele ila suala la matokeo uwanjani hilo lipo kwenye benchi la ufundi,” amesema.

Tayari jana kikosi kilianza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.