NAMNA PUMZI YA MOTO ILIVUTWA UWANJA WA MKAPA

ILE pumzi ya moto wapinzani wa Simba kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, hatua ya robo fainali Orlando Pirates waliivuta baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0, Uwanja wa Mkapa.

Wimbo wa matumizi ya nafasi zinazotengenezwa kwa Simba utadumu kwenye vichwa vyao kwa kuwa mashuti 17 waliyopiga ni matano yalilenga lango la wapinzani wao.

Kwa upande wa kona walipiga jumla ya kona 5 sawa na wapinzani wao ambao walionekana wamekuja kujilinda kwenye mchezo huo. Hapa Spoti Xtra inakuletea namna picha ilivyochezwa:-

Mikono ya Manula

Mikono ya kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula iliweza kugusa miguso 12 ndani ya dk 90 kwenye mchezo huo.

Ilikuwa ni dk ya 18,33,39,52,72,75,76,79,80,83,89 na 90. Jitihada za Orlando Pirates kuweza kumtungua zilikwama na kiongozi wao alikuwa ni John Hotto ambaye alikuwa wa kwanza kupiga shuti lililolenga lango kwa Manula dk ya 18.

Pini zilitembezwa

Licha ya kutokuwepo kwa kiungo Sadio Kanoute ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, warithi wake waliweza kuvaa viatu vyake kwa umakini.

Taddeo Lwanga alitembeza pini dk 50 hakuweza kumaliza dk 90 aliingia Rally Bwalya kuchukua nafasi yake dk ya 50, Jonas Mkude alicheza faulo dk ya 39.

Pia kiungo Pape Sakho aliweza kucheza faulo dk ya 10 na 61 iliyopelekea kuonyeshwa kadi ya njano,Pascal Wawa alicheza faulo dk ya 17.

Viungo bado kuna shida

Licha ya ushindi ambao walipata Simba inaonekana kwamba kwenye upande wa viungo bado ni tatizo hasa kwenye kutengeneza mipira kuelekea kwa washambuliaji.

Chris Mugalu ambaye alikuwa mshambuliaji wa kati alionekana akiwa hana kazi kwa kuwa hakuwa akipewa mipira mara kwa mara jambo lililomfanya kuishia kucheza faulo dk 20,40 na 73 huku akipiga shuti moja dk ya 56 ambalo lililenga lango na alitolewa dk ya 85 nafasi yake ikachukuliwa na Meddie Kagere.

VAR imekutana na mtumiaji

Ikiwa ni mara ya kwanza kuweza kutumika kwenye ardhi ya Tanzania,teknolojia ya VAR ilikutana na mtumiaji ambaye ni Bernard Morrison mzee wa kuchetua.

Faulo aliyochezewa dk ya 65 akiwa ndani ya 15 ilitosha kuweza kusimamisha mchezo kwa muda na mwamuzi kufanya mawasiliano na watu wa VAR ila mwisho wa siku maamuzi ikawa ni penalti.

Morrison alitumia dk 76 na nafasi yake ilichukuliwa na Mzamiru Yassin, kwenye dk hizo alizokuwa uwanjani aliweza kupiga jumla ya mashutimanne ambayo yalilenga lango ilikuwa dk ya 20,35,45,59.

Morrison alichezewa faulo dk ya 5 ilikuwa 18,36,58,65 na 73 na alipiga faulo dk ya 37,59,62.

Zawadi ya Pasaka

Beki kitasa Shomari Kapombe aliweza kutoa zawadi ya Pasaka kwa Watanzania na mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao kwa pigo la penalti dk ya 66 iliyomshinda kipa Richard Ofori ambaye alionyeshwa pia kadi ya njano dk ya 66.

Ukiweka kando pigo hilo la penalti, Kapombe alipewa jukumu la kupiga faulo ilikuwa dk ya 5,kona alifanya hivyo dk ya 35 na kurusha mipira ilikuwa hivyo dk ya 9,10,12.

Hawa Orlando Pirates moto

Orlando Pirates hawakuwa na presha licha ya kuwa ugenini mbele ya mashabiki 60,000 walicheza kwa kutulia.

Nkwame Pebla alikuwa anawafanya anavyotaka mabeki wa Simba kwa kuwa alisepa na kijiji dk ya 8 na kupiga shuti ambalo halikulenga lango.

Bandule Shandu alikuwa akila sahani moja na Morrison na aliweza kumdhibiti. John Hotto huyu kila eneo alikuwepo aliweza kmtibulia mipango Mugalu na Kapombe pia majukumu ya mapigo huru yapo kwenye miguu yake alipiga faulo dk ya 50 alionyeshwa njano dk ya 76.

Hazina ya Simba

Zimbwe alifanya yake na alikuwa akipanda na kushuka huku Henock Inonga akiweka ulinzi eneo lake kwa kushirikiana na Pascal Wawa.

Peter Banda anazidi kuimarika na aliweza kupewa majukumu ya kupiga kona ilikuwa dk ya 3 alichezewa faulo dk 5 nafasi yake ilichukuliwa na Kibu Dennis dk ya 79.

@Dizo_Click