PAN AFRICAN,GWAMBINA KUNANI HUKO WAUNGWANA?

KUNANI pale ndani ya Pan African moja ya timu yenye historia kwenye ulimwengu wa mpira ila ghafla kwa sasa mambo yanaonekana kwenda tofauti.

Tunaona kwamba kwenye mzunguko wa pili upepo umebadilika kwa mabingwa hawa wa ligi mwaka 1982 bado hawajawa kwenye mwendo mzuri.

Kocha aliyekuwa akiwafundisha hivi karibuni tulipewa taarifa kwamba ameshachimbishwa kisha akafuata kipa ambaye alifungwa mbele ya DTB naye safari imemkuta.

Haina maana kwamba haya ni maamuzi mabaya hapana kwa kuwa kila jambo linatokea kwa sababu na maamuzi yanapaswa kuheshimiwa lakini hapa cha msingi ni kuweza kutambua kipi ambacho kinaikwamisha timu kushindwa kwenda kwenye ule ubora wake.

Hivi karibuni iliweza kuambulia kichapo cha mabao 6-0 dhidi ya Transit Camp haina maana kwamba timu haina uwezo hapana jambo la msingi ni kuweza kuona uongozi na benchi la ufundi katika wakati huu wanaungana na kufanya yote kwa ushirikiano.

Huu ni muda wa kukamilisha hesabu ambazo zilianza kupigwa kwenye mzunguko wa kwanza hivyo ni wakati wa kufanya maandalizi mazuri na kupata kilicho bora.

Hakuna shabiki ambaye anapenda kuona timu inapoteza najua kwamba hata benchi la ufundi malengo yao ni kuona kwamba wanashinda mechi ambazo wanacheza.

Ikumbukwe kwamba kwa sasa huu ni mzunguko wa pili ambao huwa unakuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho kwa kuwa yule ambaye atapoteza mchezo huwa inakuwa rahisi kuipoteza ile ramani.

Kwenye mechi hizi na kwa namna ambavyo ushindani upo timu inapata ushindi iwe nyumbani ama ugenini kwa kuwa jambo la msingi ni maandalizi mazuri.

Ukiiweka kando Pan African pia mwendo wa Gwambina FC tangu ligi kuanza bado haujawa na ile afya ya soka la ushindani kwa kuwa bado haijafanya yale ambayo mashabiki walikuwa wanatarajia.

Jambo la msingi ambalo linatakiwa kwa sasa ni utulivu kwenye kila hatua na kila mmoja kuamini kwamba anakwenda kupata kile ambacho anastahili kwa kufanya kweli.

Hakuna timu ambayo inakwenda uwanjani ikiwa haitaki ushindi hapo ni muhimu kila mmoja akalitamua hilo wakati wa mchezo na baada ya mchezo.

Kwa mashabiki ni muhimu kuweza kuona kwamba wanajitokeza kuweza kuzishangilia timu zao lakini wasibebe matokeo mfukoni hilo lisipewe nafasi.

Kinachobeba matokeo uwanjani na maandalizi mazuri kisha wachezaji kutumia nafasi wanazozipata uwanjani kunafuata kwa kuwa ushindi lazima upatikane kwa mabao kufungwa.

Ipo wazi msimu lazima utakwisha kwa namna yoyote na mwisho wa siku kila mmoja atavuna kile ambacho amekipanda uwanjani.

Kuna suala la kushuka daraja ambalo hili haliepukiki na wengi wamekuwa wakifanya kweli kwenye mzunguko wa pili na kuwashangaza wengi hivyo muda wa kuanza kufanya hivyo ni sasa.

Kwa timu ambazo zinatoka Championship kuna kushuka tena daraja hili nalo inapaswa liwekwe akilini na zile ambazo zitafanya vizuri zitapanda.

Muda wa kurekebisha makosa upo na kitu cha msingi ni kuamini kwamba mpira unadunda na lolote linaweza kutokea.