WAKIWA Uwanja wa Mkwakwani, Tanga leo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara,Simba wameshinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union wakipata ushindi usiku kabisa kabla mchezo kukamilika.
Dakika 45 za mwanzo Simba iliweza kucheza kwa utulivu na kutengeneza nafasi nne za wazi lakini hazikuweza kuleta matunda kwao.
Ni bao la Bernard Morrison dk 40 na lilisawazishwa dk 76 na Victor Ackpan kwa shuti kali lililomshinda Aishi Manula.
Bao pekee la Simba la ushindi lilifungwa na Meddie Kagere dk 90+3.
Mchezo wa leo umeamuliwa na Kagere ambaye alianzia benchi na aliingia kuchukua nafasi ya Sadio Kanoute ambaye alikwama kuonyesha yale makeke yake.
Kipindi cha pili Coastal Union inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda ilikuja na mbinu tofauti na kuweza kuwapoteza Simba kwenye suala la kutengeneza nafasi na umiliki wa mpira.
Umakini mdogo pia kama ambavyo ilikuwa kwa Simba kipindi cha kwanza uliwaponza Coastal Union ambao walimaliza wakiwa pungufu baada ya nahodha wao Pascal Kitenge kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano.
Simba inafikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 18 na Yanga ni namba moja ikiwa na pointi 51.