YANGA YAINGIA ANGA ZA NYOTA STARS

AKICHEZA mechi mbili akiwa na kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza, straika George Mpole, tayari ameivutia Klabu ya Yanga inayotaka kumsajili kuelekea msimu ujao wa 2022/23.

Mpole mwenye mabao nane kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu akiitumikia Geita Gold, hivi karibuni alikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichocheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa zilizopo kwenye Kalenda ya FIFA.

Taarifa kutoka Yanga, zinadai kwamba, viongozi wa klabu hiyo wamefurahishwa na mwenendo wa straika huyo ambaye wanazidi kuendelea kumfuatilia zaidi kwa lengo la kumsajili. Mtoa taarifa huyo aliongeza kwamba, kama kiwango cha Mpole kikiendelea kulishawishi benchi la ufundi la Yanga chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, basi watalazimika kumtoa straika wao mmoja na kumchukua yeye.

“Uongozi wetu umedhamiria kufanya makubwa sana msimu ujao, maana huwezi kuamini, pamoja na kuwepo kwa mastraika wanne, tayari imefurahishwa na George Mpole wa Geita Gold, ambapo kama mambo hayatabadilika basi msimu ujao ataingia jangwani, huku Yusuph Athumani akitolewa kwa mkopo,” alisema mtoa taarifa huyo.

Yanga kwa sasa ina mastraika wanne ambao ni Fiston Mayele, Heritier Makambo, Crispin Ngushi na Yusuph Athuman, kati ya wote hao, Mayele ndiye anapata nafasi zaidi ya kucheza

Katika mechi hizo zilizochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan, alifanikiwa kufunga bao na kutoa asisti moja, jambo ambalo wengi wameona ni straika mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao.