ISHU YA YANGA KUMSAJILI KI AZIZ IPO HIVI

BAADA ya kuibuka kwa tetesi kuwa uongozi wa Yanga upo kwenye mpango wa kumsajili nyota wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Ki Aziz, Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Eng. Hersi Said ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambao ni wadhamini wa klabu hiyo, amefunguka ukweli wa jambo hilo.

Hersi aliweka wazi na kukubali kuwa ni kweli wamemuona nyota huyo na kukubali uwezo wake, ila ni ngumu kusema kuwa watamsajili kwa sasa kwa kuwa hawataki kukurupuka kwenye sekta hiyo na nguvu kubwa kwa sasa wamewekeza kwenye kulisaka taji la ligi kuu.

, Injinia Hersi amesema: “Ni kweli tuna idadi kubwa ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu. Hatukurupuki kuongeza mikataba, malengo yetu kwa sasa ni kombe la ligi kuu ili tupate nafasi ya kuiwakilisha nchi. “Tunatakiwa kuwa na nyota watakaotubeba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

KI Aziz ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana, tumemuona. Sisi kama Yanga tungetamani kuwa naye kwa ajili ya ligi ya mabingwa msimu ujao, lakini kwanza tufanye vizuri kwenye ligi kuu na kombe la (FA) ndio malengo yetu kwa sasa.

“Muda utafika wa usajili, tutafanya kufuru kama kawaida yetu.Sisi huwa hatukubali kushindwa, nachowaambia tu Wananchi usajili wa msimu ujao utakuwa bora mara mbili zaidi ya huu.”

Aziz K, aliibuka kuwa mchezaji bora wa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye kundi D, wakati Asec Mimosas ilipowachapa Simba mabao 3-0 na yeye kutajwa mchezaji bora wa mechi.