TAIFA STARS KAZINI LEO,FEI TOTO KUIKOSA SUDAN

KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo Jumanne kitacheza mchezo wa pili wa kirafiki dhidi ya Sudan kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 1:00 usiku, Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, amesema vijana wake wapo vizuri kukabiliana na wapinzani wao.

Mchezo huu unakuja baada ya Jumatano ya wiki iliyopita Taifa Stars kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

 Poulsen amesema: “Wachezaji wamejiandaa vizuri kimazoezi kwani tumekuwa tukiwafundisha namna nzuri ya kupata ushindi, kwetu utakuwa mchezo mzuri na tunaweza kutoka na ushindi.

“Sudan ni timu nzuri, tuiona ikicheza na Afrika ya Kati, wako vizuri katika kupeana pasi, hivyo endapo wakipewa muda wa kutosha na nafasi wanakuwa wanaumiliki vizuri mpira.

“Niwaombe wachezaji wetu haswa mabeki kukaa vema kwenye nafasi zao muda wote na kuumiliki vema mpira kwani kitendo cha kupoteza mpira kwa wapinzani ni jambo baya uwanjani.”

Kocha huyo raia wa Denmark, ameongeza kuwa, mchezo huo wa leo, unaweza kutoa majibu ya kikosi chake kipo imara kiasi gani kabla ya kuanza kwa mechi za kufuzu AFCON 2023.

Kiungo wa Stars, Feisal Salum anatarajiwa kuukosa mchezo wa leo baada ya kupata maumivu huku nahodha Mbwana Samatta akitarajiwa kuongoza kikosi kazi.