YANGA WAPANIA KUBEBA UBINGWA,MSAKO WAO UPO HIVI

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa hesabu zao ni kuweza kupata pointi tatu kwenye mechi zinazofuata za ligi ikiwa ni pamoja na mechi ijayo dhidi ya KMC inayotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.

Injinia Hersi Said amefichua siri mbili ambazo wanazitumia kusaka ubingwa msimu huu waliodhamiria huku akibainisha kuwa ni lazima wabebe taji la Ligi Kuu Bara kwa namna yoyote ile.

Hersi ametaja siri ya kwanza kuwa ni kuhangaika na mchezo unaofuata, yaani wanachowaza inakuwa ni mchezo unaofuata tu. hesabu za mchezo mmoja baada ya mwingine.

Pili, wamezungumza na wachezaji wao na kuwaambia wauchukulie kila mchezo kama fainali. Yanga ambao ndio vinara wa ligi kuu kwa sasa, watacheza dhidi ya KMC katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Machi 19 wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa kwanza katika mzunguko wa awali kwa mabao 2-0.

Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema kuwa malengo yao kwa sasa ni kuhakikisha wanapata alama katika kila mchezo unaofuata kutokana na mzunguko wa pili kuwa mgumu, jambo ambalo tayari wameshazungumza na wachezaji kwenye michezo hii ya mzunguko wa pili kuhakikisha wanaondoka na ushindi hasa katika mchezo unaofuata dhidi ya KMC.

“Kwa sasa hatufikirii kuwa tutacheza michezo mingapi iliyobaki na kuanza kuhesabu mechi ya ubingwa, ambacho tumewaambia wachezaji ni kwamba kila mchezo ni kama fainali kwetu katika huu mzunguko wa pili, hivyo ambacho tunatakiwa kufanya ni kushinda katika mchezo ambao upo karibu yetu.

“Mfano kwa sasa tunafikiria kuhusu mchezo wetu unaofuata dhidi ya KMC na wala hakuna kingine ambacho tunawaza, tunahitaji kupata matokeo mazuri katika mchezo huo ili tuendelee kukaa kileleni,” amesema kiongozi huyo.

Kwenye msimamo Yanga ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 17 na ile safu ya ushambuliaji imetupia mabao 29.