BERKANE WATAMBA KUWA NI BORA KULIKO SIMBA

NYOTA wa zamani wa kikosi cha Yanga ambaye kwa sasa anakipiga ndani ya kikosi cha RS Berkane, Fiston Abdoul Razak ameweka wazi kwamba kikosi chao ni bora kuliko wapinzani wao Simba.

Jana, Machi 10 RS Berkane waliwasili Tanzania kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa baada ya kuanza safari Machi 9 wakitokea nchini Morocco.

Kiungo huyo amebainisha kwamba mchezo dhidi ya Simba utakuwa mgumu lakini wao wanaamini kwamba ni bora kuliko Simba.

“Mchezo utakuwa mgumu ila sisi ni bora kuliko Simba, ukiangalia wengine tunapajua na tutahakikisha tunapata matokeo tunayoyataka kwenye mchezo huo.”

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Morocco, Simba ilipoteza katika dakika 45 za mwanzo kwa kufungwa mabao 2-0 na dakika 45 za kipindi cha pili waliweza kujilinda.

Hivyo wanahitaji kulipiza kisasi cha kuweza kushinda kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa,Uwanja wa Mkapa Machi 13.