HERI YA SIKU YA WANAWAKE WOTE DUNIANI

LEO ni Jumanne, Machi 8,2022 ni siku ya Wanawake Duniani, tunaungana na wale wote ambao wanaosherehekea siku hiyo.

Hapa tunaangalia baadhi ya Wanawake ambao wapo kwenye ulimwengu wa soka wakiwa ni viongozi.

Zamani ilikuwa ni nadra sana kuona mambo haya yakitokea ila kwa sasa imekuwa ni ajira na wengi wanafanya kazi ile kwa sana:-

Barbara

Septemba 5,2020 Barbara Gonzalez alitangazwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba akichukua mikoba ya Senzo Mbatha ambaye yeye yupo ndani ya kikosi cha Simba.

Ameweza kutwaa mataji 6 tofauti katika ulimwengu wa soka.

Ngao ya Jamii katika kufungua msimu wa 2020/21, Simba ilitwaa Kombe la Shirikisho kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mwisho wa reli Kigoma.

Pia Simba ilitwaa taji la Ligi Kuu Bara na kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika iliishia hatua ya Robo fainali ilipoteza mbele ya Kaizer Chiefs kwa jumla ya kufungwa mabao 4-3.

Ligi ya Wanawake kwa Simba Queens, Januari mwaka huu Kombe la Mapinduzi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC pia Simba Super Cup.

Kwa msimu huu wa 2021/22 Barbara bado yupo na timu hiyo ambayo ilitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ipo kwenye Kombe la Shirikisho hatua ya makundi.

Inapambana kutetea taji la ligi pamoja na Kombe la Shirikisho msimu huu. Kwenye ligi ipo nafasi ya pili na pointi 34 baada ya kucheza mechi 16 kabla ya mchezo wa jana.

Kwenye Kombe la Shirikisho Simba ipo hatua ya robo fainali ambapo inatarajiwa kucheza na Pamba FC baada ya droo kuchezwa na ikiwa inaweza kushinda inaweza kukutana na Yanga ama Geita Gold kwenye mchezo wa nusu fainali.

Christina

Ni mpambanaji kweli Christina Mwagala ambaye yupo ndani ya kikosi cha KMC akiwa ni Ofisa Habari wa timu hiyo yenye maskani yake pale Kinondoni.

Asilimia kubwa picha zote za wachezaji wa KMC wakiwa wanatamba wawe wamefungwa ama wameshinda huwa unakuwa ni mkono wa Mwagala ambaye yupo na timu hiyo kwa sasa.

Alianza kazi hiyo msimu wa 2020/21 alichukua mikoba ya Anwary Binde ambaye alikuwa ni Ofisa Habari wa KMC.

Mwagala amesema kuwa ni muhimu kwa Wanawake kuweza kuendelea kupambana bila kuchoka.

“Kikubwa tuzidi kupambana kila kitu kinawezekana kwenye Maisha ya sasa pamoja na kuendelea kushirikiana bila kuchoka,”.

Leen

Ndani ya Championship yupo mwanadada mmoja hivi ambaye muda wote amekuwa akitoa ushirikiano kwa Wanahabari pamoja na mashabiki wa Pan African katika kupeperusha bendera ya timu hiyo.

Anaitwa Leen Essau ambaye mbali na kuwa Ofisa Habari wa Pan Afrcan pia ni Mwandishi ndani ya Kampuni ya Global Group.

Msimu wa 2021/22 alianza kuitumikia Klabu ya Pan African na mpaka sasa anaendelea kutimiza majukumu yake.

Neno lake:”Wanawake tunaweza sio mpaka tuwezeshwe tunaiongoza nchi na tunaendelea kufanya mambo makubwa zaidi ambayo watu hawawezi kutarajia,”.

Edna

Mchapakazi wa nguvu kwenye timu ya taifa ya Tanzania, akiwa ni kocha msaidizi wa timu za taifa za Wanawake pia anainoa Klabu ya Yanga Princes.

Lema amekuwa na mwendelezo mzuri akiwa na vijana wa timu ya taifa ya Wanawake pia kwenye Ligi ya Wanawake msimu wa 2020/21 aliweza kukiongoza kikosi cha Yanga kukamilisha ligi kikiwa nafasi ya pili.

Aliwahi kuliambia Spoti Xtra kuwa kuna umuhimu wa wazazi na walezi kuwaruhusu watoto kucheza soka la Wanawake. @dizo_click