MBWANA Makata, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji yenye maskani yake Dodoma ameondoolewa katika nafasi hiyo kutokana na mwendo mbovu wa timu hiyo.
Mchezo wa mwisho kukaa kwenye benchi ilikuwa ni Februari 20 uliochezwa Uwanja wa Azam Complex na ubao ulisoma KMC 2-0 Dodoma Jiji na kufanya wapoteze pointi tatu mazima.
Ndani ya michezo mitano iliyopita, Makata alijikuta akiongoza Dodoma Jiji kuambulia pointi moja tu dhidi ya Geita Gold na kukumbana na vipigo vinne, ikiwemo vitatu mfululizo ambavyo ni kama vilikoleza kuota nyasi kwa kibarua chake makao makuu ya nchi.
Taarifa rasmi iliyotolewa, Jumatano imeeleza kuwa,”Hatua hizi zimechukuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ya timu katika mashindano mbalimbali ya msimu huu wa 2021/22,”.
Kwenye msimamo wa ligi, Dodoma Jiji ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza jumla ya mechi 15.
Kinara ni Yanga mwenye pointi 39 akiwa hajapoteza mchezo hata mmoja kwa mzunguko wa kwanza uliokamilika.