KISA WAARABU MKWANJA WAONGEZWA SIMBA

AWALI uongozi wa Simba uliwatangazia wachezaji kuwapa bonasi ya dola 100,000 (Sh mil 231) katika kila mechi watakayoshinda, lakini kutokana na ugumu wa mechi ijayo dhidi ya RS Berkane ya Morocco, matajiri wa timu hiyo wameongeza mezani dola 50,000 (Sh mil 115.5) hivyo jumla mastaa hao watavuna zaidi ya Sh mil 300.

Wikiendi hii Simba itakuwa ugenini kupambana na RS Berkane ya Morocco, kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya mchezo wao wa mwisho na US Gendarmarie ya nchini Niger kumalizika kwa bao 1-1.

Habari zimeeleza kuwa uongozi wa Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ wanadaiwa kuahidi ongezeko la dola elfu 50, kwenye bonasi ya mwanzo na kufikia dola 150,000.

“Katika siku wachezaji wamewahi kuufurahisha uongozi basi ni pamoja na  Jumapili baada ya kupata sare katika mchezo wetu na US Gendarmarie ya nchini Niger, huwezi kuamini sare hiyo sasa imewafanya kuongezewa dau la dola elfu 50.

“Kama watashinda katika gemu hiyo ni wazi sasa mastaa wetu watarudi na kitita cha maana, maana bonasi imeongezeka kuachana na ile ya awali ambayo wamekuwa wakipewa kila mechi ya kimataifa dola laki moja,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally kuzungumzia ishu hii hakupatikana.

Chanzo:Championi