MTIBWA SUGAR YAPANIA KUVUNJA REKODI YA VINARA WA LIGI

UONGOZI wa Mtibwa Sugar, umebainisha kuwa, kikosi chao kipo tayari kuvunja rekodi ya Yanga ya kutopoteza mchezo hata mmoja kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Februari 23, mwaka huu ambapo Mtibwa watakuwa wenyeji wa Yanga kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Ikumbukwe kuwa, Mtibwa Sugar wanaingia kwenye mechi hii wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo kwa mabao 3-1 pamoja na kutolewa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Coastal Union kwa kipigo cha 2-0 mbele ya Coastal Union.

Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, amesema wanafahamu kwamba mchezo dhidi ya Yanga utakuwa wa mwisho kumaliza mzunguko wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo kutokana na nafasi mbaya waliyopo kwenye msimamo, lazima wahakikishe wanapata ushindi.


“Kikosi kinaendelea 
kunolewa na Kocha Mkuu Salum Mayanga, nafahamu kuwa Kocha Mayanga ana kazi kubwa sana ya kufanya mazoezini kuelekea mchezo huu kutokana na kupoteza michezo miwili iliyopita.


“Licha ya hivyo, lakini 
morali ya wachezaji ni kubwa, wanafahamu umuhimu wa mchezo huu, hivyo najua watafuata maelekezo muhimu ya mwalimu na watafanikiwa kuyatimiza.


“Mechi hii itakuwa moja 
ya mechi kubwa ya mzunguko wa kwanza kwenye ligi kwa sababu Yanga watahitaji kuendeleza rekodi ya ya kutopoteza, wakati Mtibwa tukihitaji alama tatu kujinasua kwenye nafasi mbaya tuliyopo.


“Tunafahamu Yanga 
haijafanikiwa kupoteza mchezo wowote wa ligi kuu tangu kuanza kwa msimu huu, lakini hilo halitutishi, tutahakikisha tunawaonjesha utamu wa pilipili uwanjani, tutawaonesha maana halishi ya ushindani, nawaambia tukutane Februari 23,” amesema Kifaru.

Yanga ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 14 huku Mtibwa Sugar wakiwa nafasi ya 14 na pointi 12.