KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema kuwa kukosekana kwa wachezaji wake zaidi ya saba katika kikosi chake, kunamvurugia mipango ya ushindi kuelekea michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).
Hiyo ni baada ya kuongezeka kwa majeruhi katika kikosi chake ambao ni Mkongomani, Jesus Moloko aliyeshindwa kumalizia mchezo wa FA dhidi ya Biashara United uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Yanga katika mchezo huo iliwakosa wachezaji saba, kati ya hao ni kutokana na majeraha ambao ni Yacouba Songne, Kibwana Shomari, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Chico Ushindi, Denis Nkane, Chrispin Ngushi na Dickson Job anayetumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu.
Nabi amesema kuwa katika timu wanapokosekana wachezaji zaidi ya saba kunaharibu mipango ya kiufundi ya kocha katika kupata ushindi.
Nabi alisema kuwa kikosi chake kinakabiliwa na wachezaji wengi majeruhi, hadi unafikia wakati analazimika kuwatumia majeruhi kama ilivyokuwa kwa Moloko ambaye alimtumia akiwa ana majeraha katika mchezo.
“Ikiwa wanakosekana wachezaji wale ambao wanaanza kikosi cha kwanza maana yake ni kwamba mipango inavurugika hivyo tunajipanga kwa ajili ya mechi zetu zijazo kujua namna tutakavyofanya,”.
Mchezo ujao wa Yanga ni dhidi ya Mtibwa Sugar unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Manungu, Februari 23.