MCHEZO wa KMC FC wa Ligi kuu ya NBC Soka dhidi ya Dodoma Jiji uliopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa Jumapili ya Februali 20,2022 umehamishwa na sasa utapigwa katika Uwanja wa Azam Complex Chamanzi Jijini Dar es Salaam saa moja kamili jioni.
Kwa mujibu wa barua ya Bodi ya Ligi (TPLB) iliyotumwa jana mchana ili ieleza klabu kuwa mabadiliko hayo yanatokana na Uwanja wa Benjamini Mkapa kuwa na matumizi mengine siku hiyo ya Jumapili ya Februari 20 na hivyo kuhamishiwa Azam Complex.
Lwa mujibu wa KMC wameeleza kuwa klabu imepokea kwa mikono miwili mabadiliko hayo na kwamba mashabiki na Watanzania wote waliojiandaa kwenda kuwasapoti wachezaji Uwanja wa Benjamini Mkapa wajitokeze kwenye uwanja wa Azam Complex kama ambayo barua ya TPLB ilivyoelekeza mabadiliko ya mchezo huo.
Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amesema:”Katika kipindi ambacho timu zilikuwa mapumziko ya kupisha michuano ya Kombe la Azam Sports Federation, KMC FC haikuvunja kambi na hivyo wachezaji wote waliendelea kukaa kambini sambamba na kufanya mazoezi kutokana na mpango maalumu ambao Kocha Mkuu Thierry Hitimana alikuwa ameuandaa,”.
Mchezo uliopita KMC ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Biashara United ya Mara.