SIMBA SC, leo Jumapili inatarajiwa kuvaana na ASEC Mimosas katika mchezo wa hatua ya makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Saalam.
Huu utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Simba katika hatua hii ikiwa ni timu pekee ya Tanzania katika michuano hiyo.
Simba imekuwa na historia nzuri katika michuano hiyo ya kimataifa kwa siku za karibuni, tunaamini kuwa wataenda kufanya kweli kuanzia mchezo wa leo wakiwa Kundi D.
Tunafahamu huu utakuwa ni mchezo mgumu kwa Simba, lakini wanatakiwa kupambana kwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
Simba wanatakiwa kupambana mpaka hatua ya mwisho kwa kuhakikisha wanapata matokeo bora ili kujitengenezea nafasi ya kusonga mbele hatua ya robo fainali.
Wachezaji wanatakiwa kuingia kwa tahadhari kubwa na nidhamu katika mchezo huo kwani wapinzani wao si timu ya kuibeza.
Tunaamini kuwa Simba watautumia vema uwanja wa nyumbani kwa kupata matokeo mazuri ya ushindi ikiwa ni sehemu ya kujitengenezea mazingira ya kufikia malengo.
Watanzania na mashabiki wa soka wapo nyuma yenu Simba kuhakikisha mnafanikiwa kuipeperusha vema bendera ya Tanzania.
Hakuna kinachoshindikana. Kila la kheri Simba SC, wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.