PABLO Franco, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Simba ikiwa kundi D leo itatupa karata yake ya kwanza katika mchezo wa kimataifa unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa na timu nyingine itakazocheza nazo ni pamoja na RS Berkane ya Morocco na US Gendarmerie ya Niger.
Akizungumza na Saleh Jembe, Pablo amebainisha kwamba wapinzani ambao anakwenda kukutana nao ni imara ila watapambana kufanya vizuri na kutumia uwanja wa nyumbani kwa faida.
“Tupo nyumbani na wachezaji wanatambua kwamba huu ni mchezo muhimu,wapinzani wetu tunawaheshimu ila ambacho tunakitaka ni kupata pointi tatu ambazo zitatufanya tuzidi kurejesha hali ya kujiamini.
“Ikiwa utasema kwamba tuna tatizo katika kufunga hilo naona sio sawa kwa kuwa ikumbukwe tumetoka kushinda Kombe la Mapinduzi na tuna washambuliaji ambao ni bora katika suala la kufunga ambacho kinatokea ni hali ya kawaida kwa wanamichezo muda mwingine ni suala la kuchoka lakini haina maana hawapo bora,”alisema.
Saa 10: 00 mchezo huo unatarajiwa kuchezwa leo Uwanja wa Mkapa na mshindi atasepa na pointi tatu muhimu.
Jana wachezaji wa Simba walifanya mazoezi ya mwisho Uwanja wa Mkapa na miongoni mwa nyota ambao walikuwepo ni pamoja na Henock Inonga, Pascal Wawa, Mzamiru Yassin na Aishi Manula.