JEREMIA Juma, nyota wa kikosi cha Tanzania Prisons amesema kuwa hana mashaka na mchezo wa leo dhidi ya Simba yenye mabeki wakongwe ikiwa ni pamoja na Henock Inonga, Pascal Wawa na Joash Onyango.
Juma ni mshambuliaji pekee ambaye amefunga hat trick kwenye ligi msimu wa 2021/22 na aliwatungua Namungo FC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela.
Leo Prisons iliyo nafasi ya 16 na pointi 11 inakutana na Simba iliyo nafasi ya pili na pointi 25 zote zikiwa zimecheza mechi 13.
Juma amesema:”Hatuogopi kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Simba, tunawatambua na tunajua ni timu imara lakini tunawaheshimu kwa kuwa jambo ambalo tunahitaji ni pointi tatu.
“Uwepo wa mabeki wao wakongwe haitutishi kwani hata mimi pia kwenye ligi nipo muda mrefu na nina uzoefu wa kutosha kikubwa ni kusubiri na kuona baada ya dakika 90 hali itakavyokuwa,”.
Msimu wa 2021/22 walipokutana Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 1-1 Prisons na kuwafanya wagawane pointi mojamoja.