NAHODHA msaidizi wa Simba, Gadiel Michael amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons.
Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 25 ina kibarua cha kusaka ushindi mbele ya Prisons inayokwenda kwa mwendo wa pira gwaride.
Ikumbukwe kwamba Simba kwenye mechi tatu za ligi ilizocheza ugenini imeambulia pointi moja wakati ilikuwa ikisaka pointi tisa.
Pia safu yake ya ushambuliaji haijafunga bao lolote ndani ya dakika 270 jambo ambalo linampasua kichwa Kocha Mkuu, Pablo Franco ambaye hatakuwa kwenye benchi la ufundi baada ya kufungiwa mechi tatu.
Gadiel amesema:-“Tupo tayari kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Prisons na tunahitaji pointi tatu muhimu katika mchezo wetu muhimu.
“Tunajua kwamba ushindani ni mkubwa nasi tumejipanga kupata ushindi, mashabiki wamekuwa pamoja nasi licha ya kushindwa kupata matokeo hivyo tutapambana kwa hali na mali,”.