IMEFAHAMIKA kuwa uongozi wa Yanga umetumia Sh 50 Mil kufanikisha usajili wa mshambuliaji wa Mbeya Kwanza, Chrispin Ngushi aliyekuwa akiwindwa pia na Simba na kumpa mkataba wa miaka mitatu.
Usajili wa Ngushi mwenye mabao matatu akicheza michezo 11 ya Ligi Kuu Bara msimu huu, ni wa nne kwa Yanga
kusajiliwa kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo uliofunguliwa Desemba 16, 2021.
Wachezaji wengine waliosajiliwa na Yanga na kutambulishwa ni Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ kutoka Azam FC, Denis Nkane (Biashara United) na Aboutwalib Mshery (Mtibwa Sugar).
Taarufa zimeeleza kuwa katika makubaliano ni lazima asaini mkataba wa miaka mitatu kutokana na umri wake mdogo aliokuwa nao utakaomfanya adumu muda mrefu katika soka.
Aliongeza kuwa, dau hilo la usajili litakwenda sambamba na mshahara wa Sh 3Mil kwa kila mwezi kwa kipindi chote
atakachokuwepo Yanga pamoja na kukaa katika apartment nzuri ya kisasa.
“Haikuwa kazi rahisi kufanikisha saini ya Ngushi kutoka Mbeya Kwanza kuja Yanga, kwani kulikuwepo na
vita kubwa kutoka kwa wapinzani wetu (Simba) ambao walikuwa wakihitaji saini yake.
“Usajili wake tulifanikisha wiki moja iliyopita kabla ya kumtambulisha rasmi kwa kuachia picha zake zikimuonesha akisaini mkataba na Yanga.
“Kama uongozi tulifkia uamuzi wa kumpatia ada ya uhamisho ya Sh 50Mil pamoja na mshahara wa Sh 3Mil kwa kila mwezi sambamba na apartment ambazo tumekuwa tukiwapa wachezaji wetu wa kigeni na wale wanaotoka nje ya Dar,” alisema mtoa taarifa huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema: “Dau la usajili
ni siri kati ya uongozi wa timu na mchezaji husika, hivyo sitaweza kuzungumzia hilo.”