YANGA YAINGIA CHIMBO KUMTAFUTA MSHAMBULIAJI

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa kwa sasa upo kwenye hesabu za kumsaka mbadala wa mshambuliaji wao Yacouba Songne ambaye anatarajiwa kuwa nje kwa msimu mzima wa 2021/22.

Songne aliumia mguu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting,Novemba 2,2021 kwa sasa bado anapewa matibabu ili aweze kurejea kwenye hali yake ya kawaida.

Akizungumza na Championi Jumatatu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha alisema kuwa wanatarajia kufanya usajili mdogo kwenye dirisha dogo ili kuweza kuwa imara zaidi.

“Ikifika dirisha dongo nina amini kwamba tutafanya usajili lakini sio mkubwa sana,tuna mchezaji kama Yacouba, (Songne) huyu bado aliumia hivyo tutafanya utaratibu kumpata mchezaji mwingine ambaye atakuja.

“Unajua kikosi imara kinahitaji wachezaji wazuri na kwa namna tulivyo kila mchezaji yupo bora jambo hilo linaonekana kwani hatuna hofu tunapoingia uwanjani kucheza na timu pinzani kwa namna yoyote ile kwa kuwa kila mchezaji ana uwezo mkubwa,” alisema Mbatha.

Kwenye msimamo Yanga ipo nafasi ya kwanza na pointi 20 inafuatiwa na Simba iliyo nafasi ya pili na pointi 18 baada ya kucheza mechi nane.