ANACHOKIWAZA MUKOKO JUU YA SIMBA KIPO NAMNA HII

MUKOKO Tonombe kiungo wa Klabu ya Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ameweka wazi kuwa kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba hawana hofu yoyote watapambana kupata ushindi.

Yanga ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi saba za ligi huku wakiwa wameshinda mechi  sita na kulazimisha sare mchezo mmoja ilikuwa dhidi ya Namungo FC.

Nyota huyo ameanza kuingia kwenye mfumo wa Nabi ambapo tayari ametupia bao moja kati ya 12 yaliyofungwa na Yanga kwa msimu wa 2021/22.

Akizungumza na Saleh Jembe, Mukoko amesema kuwa wanatambua kwamba mchezo wao ujao ni dhidi ya Simba hawana mashaka zaidi ya kuomba Mungu awape afya njema.

“Kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Simba tupo tayari tunaomba Mungu atupe afya njema ili tuweze kuwa wazima siku hiyo tutakayokutana uwanjani.

“Mchezo utakuwa mgumu hilo lipo wazi lakini kikubwa ambacho tunahitaji ni ushindi kama ambavyo tumetoka kufanya mbele ya Mbeya Kwanza,” amesema.

Mchezo wa mwisho mbele ya Mbeya Kwanza kabla ya Yanga kukutana na Simba Desemba 11 ulichezwa katika Uwanja wa Sokoine na Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 na mchezo wa Simba wa mwisho kabla ya kukutana na Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold Uwanja wa Mkapa.