UONGOZI wa Yanga umesema kuwa baada ya kutoa sare katika mchezo uliopita dhidi ya Namungo hawatahitaji matokeo kama hayo katika mchezo unaofuata dhidi ya Mbeya Kwanza zaidi ya ushindi tu.
Yanga katika mchezo uliopita walitoa sare dhidi ya Namungo kwa bao 1-1, Novemba 30 wanatarajiwa kucheza dhidi ya Mbeya Kwanza mkoani Mbeya.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa matokeo ambayo waliyapata kwenye mchezo wao uliopita wanayasahau ila hawatahitaji kuyapata kwenye mchezo wao ujao.
“Mchezo uliopita tulitoka sare na Namungo, mchezo unaofuata tutacheza na Mbeya Kwanza tukiwa ugenini, hatuhitaji jambo lingine zaidi ya ushindi, Wanayanga wote pia hawahitaji matokeo mengine zaidi ya ushindi na ndio maana tunawaambia kuwa Mbeya Kwanza watatusamehe.
“Najua kila mchezo wa ligi kwa sasa ni mgumu, hivyo haitakuwa rahisi kupata ushindi lakini hilo halitatuzuia sisi kushindwa kupata ushindi, tumejiandaa vya kutosha kuhakikisha tunatimiza malengo yetu ambayo ni ushindi,” amesema Bumbuli.
Tayari kikosi cha Yanga kimeibukia Mbeya mapema kabisa leo Novemba 28 kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo wa ligi unaatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Sokoine.
Miongoni mwa nyota wa Yanga ambao wapo ndani ya jiji la Mbeya ni pamoja na Fiston Mayele, Dickson Job,Diarra Djigui,Ninja.