DIDIER Gomes, aliwahi kuwa kocha mkuu wa Simba ameweka wazi kuwa kwa namna kikosi hicho kilivyo kinaweza kupata ushindi mbele ya Red Arrows katika mchezo wa Kombe la Shirikisho.
Leo Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco itakuwa na kazi ya kusaka ushindi kwenye mchezo wa mtoano ambao utashuhudiwa na mashabiki 35,000.
Gomes amesema kuwa wachezaji wa Simba wana uwezo mkubwa na anaamini ikiwa watatulia na kufuata maelekezo ambayo watapewa watapata ushindi.
“Kikosi cha Simba kina wachezaji wazuri na wenye uwezo na imani yangu ni kuona kwamba kwenye hatua ya Kombe la Shirikisho watafanya vizuri na wachezaji wakitulia watapa ushindi mzuri.
“Benchi la ufundi ambalo nilifanya nalo kazi kwa upande wa wasaidizi ambao ni Seleman Matola na Hitimana Thiery ni watu wenye uwezo mkubwa na wanajua namna ambavyo wachezaji wanaweza kuwapa matokeo ni jambo la kusubiri na kufanya kazi kwa umakini,” amesema Gomes