KIKOSI cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco kimeendelea na mazoezi kwa ajili ya kuivutia kasi Red Arrows katika mchezo wao wa kimataifa.
Ni Novemba 28 mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa ambapo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote kusaka ushindi ndani ya dakika 90.
Simba imeangukia hatua ya Kombe la Shirikisho baada ya kuangukia pua katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa ilinyooshwa mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa na kuondolewa mazima.
Licha ya kwamba mchezo wa kwanza ugenini ilishinda mabao 2-0 imeondolewa kwa idadi ya kufungwa mabao mengi ikiwa kwenye ngome yake Uwanja wa Mkapa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtanza Mangungu amesema kuwa kila kitu kipo sawa na wanahitaji kuweza kupata ushindi kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
“Kwa sasa mwalimu anaendelea kuwapa mbinu wachezaji na nina amini kwamba kwa umuhimu wa mashindano ya kimataifa tutafanya vizuri na kupata matokeo.
“Ushindani ni mkubwa kwa kuwa kila timu ipo wazi ni imara na zina ubora hilo halitupi mashaka kwani wachezaji wetu tulionao ni imara na wana uzoefu kimataifa,”.