IKIWA Uwanja wa Uhuru, leo Novemba 21 Klabu ya Azam FC imepoteza pointi tatu mazima mbele ya KMC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Mchezo wa leo unakuwa ni wa kwanza kwa KMC kushinda ndani ya ligi kwa kuwa katika mechi tano zilizopita haikuwa inajua ushindi upoje kwa msimu wa 2021/22.
Bao la kwanza lilipachikwa na Matheo Anthony aliyemtungua Mathias Kigonya kwa shuti kali dakika ya 13 kisha kabla hawajaenda mapumziko, Azam FC waliweka usawa kwa bonge moja la shuti lulilopigwa na Charles Zulu dakika ya 43 na kipa Farouk Shikalo hakuwa na chaguo.
Kipindi cha pili ngoma ilikuwa nzito kwa timu zote mbili kupambana kupata pointi tatu na katika jitihada hizo zilimfanya winga Miraj Athuman aonyeshwe kadi ya njano kwa kuwa alipiga mpira wakati mwamuzi amepuliza kipyenga.
Ni bao la Hassan Kabunda liliwazima Azam FC ilikuwa dakika ya 89 alimalizia shuti ambalo lilitemwa na Kigonya baada ya matheo kufanya jaribio la kichwa ndani ya 18.