Home Sports MAKIPA PONGEZI MNASTAHILI,KAZI IINDELEE

MAKIPA PONGEZI MNASTAHILI,KAZI IINDELEE

KWENYE suala la kusaka ushindi uwanjani kuna wachezaji 11 ambao huwa wanapambana kwa ajili ya timu na ipo wazi ushindi unapatikana kwa ushirikiano wa kila mchezaji.

Kwa habari ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kushindwa kupenya hatua ya mtoano wa Kombe la Dunia hiyo imeisha hakuna tutakachoweza kubadili zaidi ya maumivu.

Tunajua kwamba mashabiki matumaini yao makubwa ilikuwa ni kuona kwamba timu inapenya hatua ya mtoano na kuandika rekodi tamu ya kushiriki Kombe la Dunia imebaki hadithi kwa wakati huu kwamba tuliwahi kuongoza kundi J.

Pongezi kwa wachezaji kwa namna ambavyo mlikuwa mkitimiza majukumu yenu mwanzo mwisho ila hapo kuna jambo la kujifunza kwa yale makosa ambayo mliyafanya kwa kuwa yamekuwa yakijirudia.

Kocha Mkuu, Kim Poulsen hilo aliliweka wazi baada ya timu kufungwa mabao 3-0 dhidi ya DR Congo Uwanja wa Mkapa kwenye hili hapa maumivu yalikuwa makubwa kwa kila shabiki na matumaini ya kuweza kufuzu yakayeyuka hapo jumlajumla.

Poulsen aliweka wazi kwamba tulifungwa kutokana na makosa ambayo tuliyafanya, ikumbukwe kwamba makosa hayo tuliyafanya pia tulipocheza na Benin tukafungwa bao 1-0 tena hapohapo Uwanja wa Mkapa.

Wanasema yaliyopita si ndwele basi tunapaswa tugange yajayo na imani yangu ni kwamba kuna mabadiliko yanahitajika kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi katika mbinu za kusaka ushindi.

Jitihada ambazo mlizionesha kwenye mchezo dhidi ya Madagascar hazikuwa za kawaida na ilionyesha kwamba mlikuwa mnahitaji kitu jambo ambalo liliweza kutokea.

Iwe hivyo kwenye mechi zote za mashindano kwani licha ya kugawana pointi mojamoja kwa kufungana bao 1-1 bado kulikuwa na jitihada ambazo zilionekana na wachezaji mlifanya kazi kubwa.

Weka kando hilo sasa jamvini leo nazungumzia makipa ambao wamekuwa na jukumu kubwa katika kuzuia michomo inayopigwa na wapinzani wao.

Imekuwa kawaida sana kuona tuzo nyingi wanasepa nazo wachezaji wa ndani na hasa washambuliaji huku makipa wakiwekwa kando kwenye tuzo nyingi.

Katika hili pia inapaswa litazamwa kwa kuwa moja ya sehemu ambayo imetawaliwa na wazawa kwenye ligi ya Bongo ni hapa kwenye makipa.

Ni timu kadhaa ambazo zinawatumia makipa wakigeni kuwa ni namba moja ikiwa ni pamoja na Yanga, Azam FC,Namungo lakini kwa nyingine ambazo zimebaki kipa ni mali ya mzawa.

Kuna umuhimu wa kulitazama hili eneo kwa upekee na kuwapa motisha zaidi ili wazidi kupambana kwa kufanya kazi kwa umakini ili kuzidi kuifanya hii sehemu iwe mikononi mwa wazawa ambao kesho watakwenda nje kuiwakilisha Tanzania.

Kipa kama Aboutwalib Mshery ambaye yupo ndani ya Mtibwa Sugar ni kijana ambaye ana uwezo mkubwa na kipaji kinaonekana hivyo bado ana jukumu la kupambana na kaka yake Aishi Manula katika ubora ili kuifanya kazi yake kwa ubora zaidi.

Manula anaonekana kuwa bora muda wote kwa miaka sita sasa na mrithi wake pale ambapo atapata nafasi ya kucheza nje ya Tanzania basi awe ni imara katika kutimiza majukumu yake.

Previous articleSIMULIZI YA ALIYEPUNGUZA UZITO
Next articleCHEKA, ALKASASU KUPASUANA USIKU WA MISHINDO