HAJI MANARA:NYOTA WOTE NDANI YA YANGA NI VYUMA

UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa wachezaji wote ambao wamesajiliwa na kikosi hicho kwa msimu wa 2021/22 ni vyuma vya kazi jambo ambalo linawapa tabu benchi la ufundi kwenye suala la upangaji wa kikosi.

Yanga ipo nafasi ya kwanza na pointi 15 huku safu yao ya ushambuliaji ikiwa imetupia mabao tisa na ile ya ulinzi imeokota bao moja kwenye mechi tano.

Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara amesema kuwa hakuna usajili wa maana kama ambao umefanywa wakati huu na wamesajili vyuma vya kazi kwa ajili ya kuweza kufikia malengo ambayo wamejiwekea.

“Usajili wetu ni wa vyuma vya kazi tupu yaani Yanga hii yule ambaye anaanza ni chuma na ambaye yupo benchi ni chuma hapo sasa unaanza kujiuliza benchi la ufundi lipo kwenye hali gani.

“Nadhani umeona kwamba kuna mechi ameanza yule Jesus Moloko nakwambia hapo Mukoko Tonombe hajaanza na mambo yanakwenda sawa kama hakuna kitu ambacho kimetokea, una Yanick Bangala ule ukuta wako unakuwa chuma hapo kuna mechi nyingine Bakari Mwamnyeto hakucheza.

“Ukija kwa kipa Diarra Djigui huyu usajili wake ulibezwa sasa nani anaweza kufanya kazi kama Diarra ni moja ya kipa mzuri akianza ni uhakika katika mipira yake pamoja na kuokoa michomo nawaambia mashabiki ni muda wao kujivunia ila wasivimbe,” amesema Manara.