NABI AOMBA WACHEZAJI WAPEWE ULINZI

NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kuna umuhimu wa waamuzi kuweza kuwalinda wachezaji kwenye mechi zote ambazo wanacheza.

Kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Agosti 20,2022 wakati ubao ukisoma Coastal Union 0-2 Yanga kiungo Jesus Moloko alikwama kukamilisha dakika 90.

Kiungo huyo alitoka dakika ya 25 nafasi yake ikachukuliwa na Dickson Ambundo ambaye aliweza kukamilisha dakika zilizobaki.

Sababu ya Moloko kutolewa ni kuchezwa faulo ambayo ilimsaabisha maumivu jambo ambalo limemfanya Nabi kuomba umakini kwa waamuzi kwa kila mechi.

“Unaona tumecheza mchezo wetu tukiwa na huzuni hasa baada ya kupokea taarifa kuhusu mashabiki zetu tunawapa pole familia hili ni jambo gumu lakini limetokea tunaamini kwamba mpira unategemea mashabiki na niliwaambia wachezaji wacheze kwa umakini mkubwa.

“Kwa upande wa waamuzi nina amini kwamba wanaona namna kazi ilivyo hivyo sio kwa mechi za Yanga pekee hapana bali kila mechi ni muhimu kuwa makini ili kuweza kuwalinda wachezaji kwani hawa wanafamilia pia na wanafanya kazi ili waweze kuzitunza.

“Ikiwa wataumia kazini itakuwa ngumu kwao kwenye kutimiza majukumu yao na mchezaji ambaye anacheza faulo pia na yeye ipo siku ataumizwa hili sio jambo la mpira lazima kila mchezaji awe makini na waamuzi nao wawalinde wachezaji,” amesema.