TAMBO kwa sasa kwa zinazidi kutawala ambapo kila mmoja anaamini kwamba amefanya usajili mzuri na anaweza kuchukua kila kitu ambacho anakihitaji.
Ipo hivyo na ni maisha ya mpira hakuna anayeweza kuzuia maneno ambayo yanatokea lakini ukweli unabaki ukweli kwamba mpira unahitaji vitendo zaidi.
Yale maneno ambayo yamekuwa yakitolewa na mashabiki pamoja na viongozi yana muda wake ambao utakwisha hasa vitendo vikianza kutenda kazi.
Sasa kwa nini muda huu tambo ziwe nyingi wakati muda unakuja wa kujua mbichi na mbivu? Basi acha tusubiri na kuona nini ambacho kitatokea.
Msimu uliopita kila mmoja alikuwa na mipango yake na mwisho wa siku alivuna kile ambacho alipanda hivyo muda unakuja tena wa kuvuna kile ambacho kila mmoja atapanda.
Kwa wiki hii ndani ya Agosti kuna matukio mengi kuhusu matamasha hapo picha la msimu ujao linaanza kuchorwa hivyo mipango ni muhimu.
Kwa wachezaji tuna amini kwamba maandalizi ambayo mmeyafanya yatakuwa na mwendo wa kutoa majibu hivyo kazi ni kwenu kutimiza majukumu ambayo mtapewa.