RAIS MPYA ANATAKA KUWEKA REKODI YA CAF JANGWANI

RAIS wa Klabu ya Yanga,Injinia Hersi Said ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo ametoa ahadi ya kuweka rekodi ya kuifanya Yanga kuwa timu ya kwanza kubeba ubingwa wa Caf.

 Yanga imebeba mataji matatu  msimu wa 2021/22 ikiwa ni Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na Ngao ya Jamii, inatarajiwa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Hersi amesema kuwa anataka kuona ndani ya kipindi cha uongozi wake analeta Kombe la Caf.

Hersi amesema kuwa hilo linawezekana kwake kutokana na mikakati atakayoiweka ikiwemo kusuka kikosi imara cha wachezaji bora wa kiwango kizuri.

“Ninataka kuona timu yetu ya Yanga inaweka rekodi ya kwanza ya kubeba ubingwa wa Afrika na hilo linawezekana kwetu.

“Nafahamu hivi sasa kila timu itaiangalia Yanga kimataifa kutokana na usajili ambao tumeufanya wa kutikisa Afrika, tukiwa tumetoka kuwatangaza wachezaji  ikiwa ni Morrison (Bernard) na Kambole (Lazarous),” amesema Hersi.

Pia baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo Yanga Julai 9,2022 iliweza kumtangaza Gael Bigirimana kuwa ingizo jipya ndani ya kikosi cha Yanga.