ULIKUWA ni msimu mzuri kwa kila mmoja na mashabiki wameona hali halisi hasa maana ile ya mpira kuchezwa kwa ushindani na uwazi ndani ya dk 90.
Suala la kushuka daraja na bingwa hilo limeweza kuwa miongoni mwa taarifa ambazo zipo mikononi mwa familia ya michezo kwa wakati huu.
Champioship imeshatoa timu zake mbili ambazo zitashiriki ligi msimu ujao kwa kuwa hawa kazi yao waliimaliza mapema tena kwa ushindani mkubwa.
Zilizokamilisha mwendo kwa ushindi zina tiketi mkononi kuweza kushiriki ligi msimu ujao na zinapashana na zile mbili kutoka kwenye ligi baada ya kupata kibali cha kushiriki Championship.
Kila sehemu mambo hayakuwa mepesi ni magumu kuanzia uwanjani mpaka nje ya uwanja ushindani ni mkubwa kwani hakuna ambaye alikuwa anakwenda kinyonge uwanjani.
Jambo la msingi ambalo limetokea kwa msimu wa 2021/22 ni somo kwa ajili ya msimu ujao kwa kila timu bila kujali ni nafasi ipi imeweza kumaliza.
Yote kwa yote zipo ambazo zimepanda ndani ya ligi ikiwa ni pamoja na Ihefu pamoja na DTB ambayo kwa sasa inaitwa Singida Big Stars wanastahili pongezi kwa hatua kubwa waliyoifikia..
Pia zipo ambazo zimebaki ndani ya Championship hizi nazo malengo yao ni kuona zinaweza kuibuka kwenye ligi kuu wakati mwingine baada ya msimu huu mambo kuwa magumu kwao.
Yote haya yanatokana na ushindani ambao ulikuwa upo ndani ya ligi,kila mechi kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi ilikuwa ni fainali.
Kwa upande wa Ligi ya Wanawake Tanzania nao hawakuwa nyuma wamefanya kazi kubwa katika kuyatafuta mafanikio na kila mmoja akavuna kile ambacho alikuwa anahitaji.
Wapo ambao walianza na malengo ya kuhitaji kutwaa ubingwa lakini mwisho wa siku ni pointi ziliwagomea hivyo muda uliopo kwa sasa ni kujipanga upya.
Ipo wazi kuwa suala la uwekezaji hasa kwa wadhamini upande wa Ligi ya Wanawake pamoja na ile Championship wengi wamegeuka pembeni.
Kwa namna ambavyo mechi zao zimekuwa na ushindani kuanzia kwenye Ligi ya Wanawake pamoja na Championship wamekuwa wakionyesha kwamba uwekezaji ukiwepo huku pia ushindani utakuwa ni mara dufu.
Bado nina amini kwamba wengi wameona namna hali ilivyo na kwa msimu ujao basi kutakuwa na maboresho makubwa pamoja na kuongezeka kwa ushindani zaidi.
Tukirudi kwenye ligi kuu mbili zimeshuka jumlajumla ambapo ni Biashara United na Mbeya Kwanza huku mbili zikiwa kwenye mchezo wa mtoano Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.
Suala kubwa ni kwenye mipango na kufanya yote kwa umakini kwa kuwa huwezi kukwepa kushuka wala huwezi kuepuka kupanda ikiwa umejipanga vema.
Zenye nafasi ya kucheza mtoano bado zina nafasi ya kujinasua hapo zilipo kwa kusaka ushindi kwenye mechi zao watakazocheza na ikiwa watashindwa basi watakuwa kwenye maisha mapya ndani ya Championship.
Kwa zile ambazo zimeweza kufikia malengo yao pongezi na ziwe juu yao na kwa zile ambazo zimeshindwa kufikia malengo ni lazima kutazama pale ambapo walishindwa kufanya vizuri msimu huu.
Kikubwa ni kufanya kazi kwa juhudi na kujipanga kwa msimu ujao kwa kuwa hesabu za msimu huu zimefika ukingoni na msimu ujao nao utakuja kwa namna yoyote ile.
Kila la kheri wanafamilia ya michezo kwenye kukamilisha malengo ya wakati ujao na muhimu kuamini kwamba ushindani mkubwa unaongeza ubora wa ligi.