JANA asubuhi sana Simba ilimshusha winga wa kimataifa raia wa Kenya, Harrison Mwendwa kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumsajili kuelekea katika msimu ujao.
Simba tayari imefanikisha usajili wa kimyakimya wa wachezaji wanne pekee ambao ni Mzambia, Moses Phiri aliyetambulishwa tayari wengine Mnigeria Victor Akpan, Mghana Augustine Okrah na Nassoro Kapama.
Timu hiyo inaendelea kufanya usajili wa kimyakimya katika baadhi ya maeneo kwa hofu ya kuingiliwa na wapinzani wao, Yanga.
Championi Jumamosi, lina uhakika wa ujio wa winga huyo aliyetua asubuhi ya jana kwa ajili ya kufanya mazungumzo na uongozi wa Simba kabla ya kusaini mkataba.
Taarifa ambazo imezipata gazeti hili, upo uwezekano mkubwa wa winga kusaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo, kama mazungumzo yakifikia pazuri kati ya menejimenti yake na Simba.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa winga atasaini mkataba wa muda huo kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika wa kuichezea Klabu ya Kabwe Warriors ya Zambia.
Aliongeza kuwa winga huyo mara baada ya kutua nchini, haraka aliopokelewa na baadhi ya viongozi wa Simba na kupelekwa kwenye moja ya hoteli kubwa tayari kwa ajili ya kufanya mazungumzo hayo.
“Mwendwa amewasili nchini asubuhi ya leo (jana) akitokea mapumzikoni nchini kwao Kenya baada ya Ligi ya Zambia kumalizika akicheza katika klabu ya Kabwe Warriors.
“Na ametua kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kusaini mkataba baada ya Simba kuonyesha nia ya kuhitaji saini yake.
“Simba ilikuwa ikimfuatulia kwa muda mrefu Mwendwa, hivyo msimu huu ndio tumeona muafaka kwetu kumsajili baada ya mkataba wake kumalizika huko Kabwe,” alisema mtoa taarifa huyo.
Championi tulimtafuta Mwendwa ili azungumzie ishu alisema kwa kifupi: “Ni kweli nipo Dar, lakini tutazungumza zaidi baadaye.”
Mtendaji Mkuu (C. E.O) wa Simba, Barbara Gonzalez hivi karibuni alizungumzia usajili kwa kusema kuwa: “Tumepanga kufanya usajili wetu wa kimyakimya kwa hofu ya kuingiliwa na timu nyingine, kwani mara kadhaa tumekuwa tukifutilia mchezaji na klabu nyingine kubwa kuingilia zikiwemo za hapa nyumbani.”