BEKI wa zamani wa Chipa United, Frederic Nsabiyumva raia wa Burundi ‘Beki Katili’ ameweka wazi kwa kusema ataweka wazi ujio wake ndani ya Simba baada ya kukamilisha kila kitu kwa kuwa mambo yake anapenda kuyafanya kwa usiri mkubwa.
Nsabiyumva ambaye aliachwa na Chipa United ya Afrika Kusini, kwa sasa bado anafanya mazoezi na timu ya Jomo Cosmo ambayo ipo chini ya meneja wake, Jono Sono wa Afrika Kusini.
Mrundi huyo mwenye miaka 27 ambaye ni mwili jumba amekuwa akisifika nchini Burundi kama mmoja kati ya mabeki wa kali kutokana na uwezo mkubwa wa kukaba katika nafasi ya beki wa kati.
Beki huyo ambaye alikuwepo hapa nchini hivi karibuni na timu ya taifa ya Burundi ambayo ilitumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mchezo wake wa kuwania kufuzu AFCON 2023 dhidi ya Cameroon.
Akizungumza na Championi Jumatano, Nsabiyumva alisema kuwa ujio wake Simba utakuwa wazi ikiwa baada ya kila kitu kuwa sawa lakini kwa sasa bado yupo Afrika Kusini akiendelea na maisha yake.
“Nipo Afrika Kusini naendelea na mambo yangu mengine ila suala la kuhusu kuja Simba nadhani ni jambo la muda tu kwa sababu kila kitu kikiwa tayari kitakuwa wazi na huwa napenda kuweka wazi mambo yakiwa yamekamilika.
“Siwezi kuongeza jambo lingine kwa sababu tunatakiwa kuacha muda ufanye kazi halafu tutaweka wazi maana natambua kwamba Simba ni timu kubwa na imekuwa ikifanya vizuri katika michuano mikubwa, kuhusu wachezaji wa Kirundi kucheza huko nawaona ila siwezi kuweka chochote kwa sasa,” alisema Nsabiyumva.