YANGA YASHUSHA MAJEMBE MAWILI KWA MPIGO

IMEFICHUKA kuwa, mabingwa wa Ligi Kuu Bara 2021/22, Yanga SC, imewashusha kimyakimya jijini Dar es Salaam mastaa wao wawili wapya ambao ni mlinzi wa kimataifa wa DR Congo, Joyce Lomalisa na mshambuliaji wa kimataifa wa Angola, Adriano Belmiro Duarte Nicolau ‘Yano’ kwa ajili ya kukamilisha usajili wao.

Taarifa kutoka chanzo chetu cha kuaminika ndani ya Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, mastaa hao walitarajiwa kutua nchini jana Jumamosi usiku kwa siri kubwa kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo na mabosi wa Yanga na kusaini mikataba ya kuitumikia timu hiyo kuelekea msimu ujao.

 

“Ni kweli leo (jana Jumamosi) tunatarajia wachezaji wetu wawili ambao tupo kwenye mazungumzo nao ambao ni beki Mkongo Joyce pamoja na yule straika wa Angola Yano watakuja hapa nchini kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho na uongozi na kukamilisha taratibu za usajili.

“Jambo hili limefanywa kwa siri kubwa na huenda ratiba hiyo ikawa na mabadiliko kidogo kutokana na mpango wa uongozi kuhakikisha hawapigwi bao na watani zetu ambao wamekuwa wanatufuatilia kwa wachezaji tunaotaka kuwasajili.”

Akizungumzia mipango yao ya usajili, Msemaji wa Yanga, Haji Manara, hivi karibuni alisema: “Tutasajili wachezaji wasiozidi watano kutoka Angola, Afrika Magharibi, Afrika Kusini na mchezaji kutoka ligi mojawapo ya Afrika Mashariki.”

Yanga inaendelea kufanya maboresho ya kikosi chao kuelekea msimu ujao ambapo mpaka sasa tayari wamefanikiwa kukamilisha usajili na kumtangaza mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia aliyemaliza mkataba Kaizer Chiefs, Lazarous Kambole.

WAANDISHI: MUSA MATEJA, IBRAHIM MUSSA NA JOEL THOMAS