BEKI WA YANGA KUIBUKIA AZAM FC

IMEELEZWA kuwa Klabu ya Azam ipo katika mazungumzo na aliyewahi kuwa Beki na Nahodha wa Yanga, Lamine Moro kwa ajili ya kuimarisha safu yao ya ulinzi msimu ujao wa 2022/23.

Beki huyo kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Newroz SC ya nchini Iraq aliyojiunga nayo Januari mwaka huu kumalizika.

Ikumbukwe kuwa, raia huyo wa Ghana alicheza kwa mafanikio makubwa ndani ya Yanga kwa kipindi cha misimu miwili, yaani 2019/20 na 2020/21.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa mtu wa karibu na mchezaji huyo, kimeeleza kuwa, tayari Azam wameanza mazungumzo na mlinzi huyo ili kuimarisha kikosi chao.

Taarifa hizo ziliendelea kubainisha kwamba, wakati mazungumzo ya beki huyo na Azam yakiendelea kuna timu nyingine Bongo zinahitaji saini yake.

“Ni kweli mabosi wa Azam wamekuwa na mazungumzo ya muda mrefu sasa kuhitaji huduma ya Lamine Moro, bila shaka ni kwa sababu alionesha uwezo mzuri akiwa na Yanga katika kipindi anacheza Tanzania. Kama mambo yataenda vizuri basi mtamshuhudia akiwa na Azam msimu ujao,” .

Akizungumzia mikakati ya usajili wa kikosi chao, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam, Zakaria Thabith, hivi karibuni alisema: “Muda wa usajili bado, kwa sasa tunapambana kushinda michezo iliyosalia katika Ligi Kuu Bara.”

Imeandikwa na Dizo Click