MASHINE MPYA YANGA HII HAPA KUTOKA ANGOLA

UNAKUMBUKA uongozi wa Yanga ulisema kuwa kuna mchezaji aliyecheza Ligi ya Angola atasajiliwa na Yanga msimu huu? Sasa ni wazi kuwa klabu hiyo tayari imemelizana na straika huyo anayefahamika kwa jina la Adriano Belmiro Duarte Nicolau ‘Yano’ anayekipiga Petro Luanda ya nchini humo.

Yano Belmiro mwenye umri wa miaka 29, katika michuano ya kimataifa msimu wa 2021/22 akiwa na Petro Luanda kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika alicheza michezo 12 na kufanikiwa kuifungia timu hiyo mabao 3 akiwa na wastani wa kufunga kila baada ya dakika 457.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Transfermarkt unaodili na thamani za wachezaji, unaonyesha kuwa kwa sasa Yano anayetumia zaidi mguu wa kulia anapatikana kwa dau la dola 325,000 (Sh mil 754.6). Sasa inaamanisha ujio wa Yano atacheza namba tisa na Fiston Mayele namba 10.

Yanga kupitia kwa msemaji wa timu hiyo, Haji Manara, hivi karibuni aliweka wazi timu hiyo kupitia dirisha kubwa la usajili itafanya usajili wa wachezaji wasiozidi watano na wasiopungua wanne wa kimataifa.

Aidha pia aliongeza kuwa, katika usajili wa wachezaji hao mmoja amecheza katika ligi ya Afrika Mashariki, mwingine ligi ya Afrika Kusini, pia yupo aliyecheza ligi ya Angola ambaye ndiye Yano.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo limezipata Gazeti la Championi Jumatano ni kwamba, Yanga tayari imemalizana na Yano Belmiro mwenye urefu wa mita 1.80 kutoka katika Klabu ya Petro De Luanda ya Angola na atajiunga na timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara na fainali ya Kombe la Azam Sports maarufu kama Kombe la FA.

“Yanga ni kweli wamemalizana na Yano kutoka katika Klabu ya Petro De Luanda ya nchini Angola. Yano ni moja ya sajili ambazo Yanga walimalizana nazo mapema kwa ajili ya kuhakikisha wanafanya vyema katika michuano ya kimataifa msimu ujao.

“Ukiangalia na yeye ana uzoefu mkubwa sana katika michuano hiyo jambo ambalo limepelekea Yanga kumsajili mshambuliaji huyo, atajiunga rasmi nadhani ni kipindi cha maandalizi ya msimu ujao ‘pre season’ atakuwa sehemu ya timu,” kilisema chanzo hiko.

Wachezaji ambao wanahusishwa kusajiliwa na Yanga mpaka sasa ni Bernard Morrison aliyecheza ligi ya Afrika Mashariki, Aziz Ki kutoka ligi ya Ivory Coast, Lazarous Kambole raia wa Zambia aliyekuwa akikipiga Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Yano Belmiro wa Angola.