MAJEMBE HAYA MAWILI KUIBUKIA YANGA

IMEELEZWA kuwa mabosi wa Yanga wamemalizana na nyota wawili kwa ajili ya msimu ujao wa 2022/23 kwenye ligi na mechi za kimataifa.

Ni Stephan Aziz KI ambaye ni mali ya ASEC Mimosas yeye ni kiungo mshambuliaji na Lazarous Kambole kutoka Kaizer Chiefs yeye ni raia wa Zambia ambaye ni mshambuliaji.

Sababu kubwa ya kuweza kunasa saini za nyota hao ni kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho ambacho kinahitaji kufanya vizuri kwenye mechi za kimataifa.

Jana, mshambuliaji wa Yanga, Yacouba Songne aliibuka Uwanja wa Mkapa akiwa na jezi iliyoandikwa jina la Aziz KI hivyo inaonesha kwamba tayari Aziz KI ni njano na kijani limebaki suala la kutambulishwa tu.

Yacouba na Aziz KI ni marafiki hasa kwa kuwa wote wanatokea nchini Burkina Faso.

Yanga inahitaji kuanza maandalizi zaidi kwa ajili ya mechi za kimataifa na inahitaji kukamilisha usajili mapema ili waweze kupata siku 30 kwa ajili ya maandalizi.