HUYU HAPA ANATAJWA KUWA KOCHA MPYA SIMBA

INAELEZWA kuwa mabosi wa Simba wapo kwenye mazungumzo na Stuart Baxter aliyekuwa Kocha Mkuu wa Kaizer Chiefs  Kabla ya kufungashiwa virago vyake huko ili aweze kubeba mikoba ya Pablo Franco.

Kwa sasa Simba ipo kwenye mchakato wa kusaka kocha mpya ambapo CV zinatajwa kuwa zaidi ya 100 mezani kwa mabosi hao ambao wapo kwenye hatua za mwisho kuweza kuachia ubingwa wao wa ligi kwa watani zao wa jadi Yanga.

Pablo alifutwa kazi Mei 30,2022 ikiwa ni siku chache akitoka kupoteza matumaini ya timu hiyo kuweza kutwaa taji la Kombe la Shirikisho ilipoweza kufungwa bao 1-0 mbele ya Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, Uwanja wa CCM Kirumba.

Habari zimeeleza kuwa mazungumzo na Baxter yamefika katika hatua nzuri hivyo ni suala la kusubiri kuona dili hilo litafikia wapi.

“Mazungumzo na kocha mpya kwa upande wa Simba yamefika hatua nzuri kwani ambacho wanahitaji Simba ni kuweza kumpata kocha mapema ili aweze kufanya usajili pamoja na kuandaa kikosi kwa msimu ujao,” ilieleza taarifa hiyo.

Ahmed Ally, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba, hivi karibuni aliweka wazi kuwa mchakato unaoendelea kwa sasa ni kusaka kocha mpya kupitia CV ambazo zimeweza kutumwa.