LICHA ya kuanza mazoezi ndani ya kikosi cha Simba kiungo Clatous Chama bado hajawa fiti kutokana na kukaa nje kwa muda mrefu akitibu majeraha ya enka.
Nyota huyo wa Simba kwa sasa yupo Bongo baada ya kurejea kutoka Zambia Julai 10 ambapo alikuwa huko akipewa matibabu ya enka ambayo aliiumia kwenye mchezo wa dabi dhidi ya Yanga.
Jana,Juni 11 Chama alianza mazoezi kwenye Uwanja wa Mo Arena akiwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi ya mechi zao zijazo za ligi.
Matola amesema kuwa kutokana na kutokuwa kwenye mazoezi kwa muda mrefu kunamfanya asiweze kuwa fiti moja kwa moja hivyo anahitaji muda kuweza kurejea kwenye ubora wake.
Matola amechukua mikoba ya Pablo Franco ambaye alichimbishwa ndani ya kikosi hicho Mei kutokana na kushindwa kufikia malengo ya timu ikiwa ni pamoja na kutwaa Kombe la Shirikisho baada ya kuondolewa na Yanga hatua ya nusu fainali, Mei 28 ambapo Simba ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Mtupiaji wa bao la ushindi alikuwa ni Feisal Salum aliyefunga bao hilo akiwa nje ya 18.
Mbali na kuwa Zambia kwa ajili ya matibabu pia Chama alikuwa kwenye kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha mkewe Mercy Chama aliyetangulia mbele za haki Mei mwaka jana.