GEORGE MPOLE: UFUNGAJI BORA NI SUALA LA MUDA TU

STRAIKA mzawa ambaye anafanya vizuri kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara, George Mpole anayekitumikia kikosi cha Geita Gold, amefunga mabao 14 msimu huu.

Mpole alijiunga na Geita Gold mwanzoni mwa msimu huu akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Polisi Tanzania kumalizika ambapo huko hakuwa na wakati mzuri.

Spoti Xtra limefanya mahojiano na Mpole kufahamu siri kubwa ya mafanikio yake msimu huu ni ipi sambamba na kuhusishwa kuwaniwa na Simba na Yanga.

Nini siri ya mafanikio yako msimu huu?

“Siri ya mafanikio yangu ni kujituma na nidhamu katika kazi, bila ya kusahau kuishi pamoja na wenzangu vizuri kwenye timu, kuwasikiliza makocha kufuata kitu gani ambacho naagizwa kukifanya uwanjani.

“Hicho ndicho kitu ambacho kimenifanya niwe vizuri zaidi kwa msimu huu.

Polisi Tanzania hukuwa na wakati mzuri, kipi kilikukwamisha?

“Mimi ni mtu ambaye huwa naamini katika kujifunza, nilivyokuwa kule nilikuwa najifunza baadhi ya vitu kwa hiyo nilikuwa najaribu kuangalia ni vitu gani ambavyo vilikuwa vinanikwamisha, lipi zuri niendelee nalo na lipi baya ambalo linafanya nisifike sehemu ambayo nataka, sasa hivi nimejaribu kurekebisha nimeona naendelea vizuri

“Siwezi kusema kwamba nilivyokuwa Polisi Tanzania nilikuwa sipati nafasi na huku Geita napata nafasi kubwa ndio maana nafanya vizuri, hapana, bali naamini katika kujifunza. Nilivyokuwa Polisi kuna baadhi ya vitu nilikuwa sivifanyi vizuri hivyo nimevichukua na kuvifanyia marekebisho.

Malengo yako ni yapi msimu huu?

“Malengo ni kuisaidia timu yangu ya Geita Gold kushika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi na isiweze kutoka katika nafasi hizo.

“Malengo yangu binafsi kwa msimu huu nifanye vizuri zaidi ikiwezekana niweze kutimiza yale ambayo nimeyapanga ya kucheza mpira wa kulipwa nje ya Tanzania.

Ndoto ya ufungaji bora kwa msimu huu ipoje kwako?

“Siwezi kuzungumzia sana kwa sababu mechi bado ni nyingi, siwezi kusema labda mimi naweza nikawa mfungaji bora au nisiwe.

“Nazidi kumuomba Mungu niendelee kuwa salama kila nitakapopata nafasi nipambane kufunga najua ninapofanya vizuri na timu yangu inafanya vizuri, hivyo ufungaji bora ni suala la muda.

Kuna ugumu gani unaupata kushindana na Fiston Mayele?

“Washambuliaji wenzangu wanapofunga mimi nawaombea waendelee kufanya vizuri kwani pale wanapofanya vizuri wananipa chachu ya kufanya vizuri zaidi wakinipa changamoto.

Geita Gold haikuwa na mwenendo mzuri mwanzoni, tatizo lilikuwa wapi? 

“Geita Gold ni timu changa kwani ni msimu wake wa kwanza kwenye ligi kuu, ni timu ambayo ina presha kubwa ukizingatia na ratiba ambayo tulipangiwa ilikuwa ngumu kwetu, kwa hiyo ilipelekea tuanze ligi vibaya.

“Tunashukuru viongozi wetu waliongeza watu kwenye dirisha dogo na tukapambana mpaka hapa tulipofikia.

Unajifunza nini kwa Reliants Lusajo ambaye pia ni straika mzawa anayefanya vizuri?

“Ni kweli mimi najifunza vitu kwa washambuliaji wengi na sio Lusajo tu bali kwa wazawa wote kwani hiyo inatusaidia hata kwenye timu yetu ya taifa tuwe na washambuliaji wazuri.

Kitu gani ambacho kilikujia kichwani ulipoitwa timu ya taifa mara ya kwanza?

“Lilikuwa jambo kubwa sana, jambo la heshima na liliongeza kitu kwenye maisha yangu ya soka kwa sababu sio kila mtu anapata nafasi ya kuitwa kwenye timu ya taifa, nilijisikia faraja sana ila napenda kuwashukuru familia yangu kwani wananiombea sana.

“Naamini kuna kitu nilikionesha watu walikiona na ndio maana nikaitwa kwenye timu ya taifa na nilisema nitakapoenda nikipata nafasi hata dakika moja nitaonesha kile kitu ambacho watu wanaamini kuwa ninacho.

Umekuwa ukihusishwa na klabu za Simba na Yanga, walishakutafuta kukuhitaji? 

“Kwa sasa siwezi kulizungumzia ila naamini wakati utakapofika mambo yote yatakaa sawa na itajulikana, kwa sasa naangalia zaidi mechi zilizobaki niweze kuisaidia timu yangu ili kuwa katika nafasi nzuri.

Mchezaji gani ambaye unamkubali kwa Tanzania?

“Kwa Tanzania sijawafuatilia sana wachezaji wote lakini nje ya Tanzania ni Ronaldinho ambaye huwa ananifanya nipende kucheza mpira.

Ni ligi gani ambayo unatamani kucheza?

“Uingereza ndio ligi ambayo naipenda na natamani sana kucheza, nina imani nikipata nafasi nitacheza.

Jambo gani ambalo hutalisahau kwenye maisha yako ya soka?

“Jambo ambalo sitakaa nilisahau kwenye maisha yangu ya soka nakumbuka nilipewa pikipiki na mshabiki kwenye mchezo wa ndondo.

“Ilikuwa Mbeya, lakini sikumbuki ni mwaka gani. Ile pikipiki ipo na naitumia kwa ajili ya kuchukulia mbolea na kazi ndogondogo za nyumbani,” anamaliza Mpole.

17 Amehusika kwenye mabao 17 katika Ligi Kuu Bara msimu huu akifunga 14 na asisti tatu.01

Huu ni msimu wa kwanza Geita Gold kushiriki Ligi Kuu Bara.

05

Geita Gold inashika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na alama 35 baada ya mechi 25.