KWENYE upande wa ukuta taratibu Tanzania inazidi kuwa imara ambapo kwenye timu ya taifa uhakika uwepo wa Bakari Mwamnyeto,Shomari Kapombe na Mohamed Hussein huku ngoma nzito ikiwa upande wa washambuliaji.
Wakati tatizo la ushambuliaji likitafutiwa tiba,kuna kijana mwingine wa kazi katika eneo la ulinzi anaitwa Dotto Shaban yupo zake ndani ya kikosi cha Tanzania Prisons.
Nyota huyo ameweka wazi kwamba lengo namba moja ni kuona timu hiyo inabaki kwenye ligi licha ya kuwa kwenye mwendo usiopendeza huyu hapa:-
“Kweli hatukuanza vizuri kwenye mechi za mwanzo hasa ukizingatia kwamba kila timu inajipanga kupata pointi tatu na yote ni matokeo ambayo tulikuwa tunapata.
“Pia hata aina ya mechi ambazo tulikuwa tunacheza zote zilikuwa ni ngumu hivyo kukosa matokeo kulitufanya tuwe kwenye mwendo ambao hatukuupenda.
“Hilo liliweza kuonwa na benchi la ufundi liliweza kufanyia kazi na kuna mechi tulikuwa tunapata matokeo nab ado tunapambana.
Kwa nafasi ambayo mpo kuna nafasi ya kubaki kwenye ligi?
“Nafasi bado ipo unajua ukiziangalia timu ambazo tunacheza nazo kisha na namna msimamo ulivyo tofauti yake sio kubwa na kila mmoja anaifikia.
“Ambacho tumekubaliana kwa sasa kwa mechi ambazo zimebaki kuweza kutulia na kufanya vizuri kwa kupata matokeo hilo linatufanya tuweze kubaki kwenye ligi na hilo ni moja ya lengo letu kubwa.
Ushindani wa msimu huu na uliopita tofauti ipoje?
“Naona msimu huu ushindani umekuwa ni mkubwa tofauti na msimu uliopita kwani uwekezaji umekuwa mkubwa na timu zilifanya usajili mzuri.
“Kila mechi ambayo sisi tunacheza ni fainali kwani hakuna timu ambayo tulikuwa tunacheza nayo mchezo unakuwa wa kawaida.
Malengo yako yapoje?
“Kwangu mimi siwezi kujitanguliza ila ninaanza na timu kwanza kikubwa ni kubaki kwenye ligi hilo ni jambo la kwanza na tunashirikiana kuweza kulitimiza.
“Baada ya hilo sasa mimi binafsi ni kuweza kufanya kazi kwa juhudi bila kuchoka katika kutimiza majukumu yetu na hilo lipo kila siku.
“Ninapenda kuweza kucheza siku moja kwenye timu ya Taifa ya Tanzania ya wakubwa na hiyo ni muhimu kwa ajili ya kulitumikia taifa letu,jambo hilo lipo na Imani yangu siku moja itawezekana.
Ikiwa mmepoteza ama kushinda muda wa mapumziko mnaambiwa nini?
“Hapo inategemea na mchezo na mbinu ambazo tumeingia nazo katika mechi, kwa mfano tukishinda tunakwenda na mbinu ya kujilinda zaidi na kushambulia.
“Tukipoteza mwalimu amekuwa akituambia kwamba makosa ambayo tumefanya ni kwa sababu ipi,hilo limekuwa likitokea na tumekuwa tukifanya kazi kwa kusikiliza benchi la ufundi.
Umecheza na Yanga na Simba,tofauti yao ipo wapi?
“Kucheza na hizi timu kubwa kwanza zote zina presha na hakuna tofauti ila zikiwa Uwanja wa Mkapa hapo kunakuwa na mashabiki wao wengi ambao wanashangilia mwanzo mwisho.
“Katika upande wa uchezaji kila timu inakuwa na mbinu zake lakini wagumu kukabika kwa sababu kila unapomaliza kazi ya kumkaba mchezaji huyu anakuja mwingine katika eneo hilo.
Ratiba yako kwa siku ipoje?
“Ratiba kubwa ni ile ambayo inafanywa na timu kwa kuwa siishi nyumbani bali ninaishi kambini,huku ni sehemu ambayo tunakuwa na ratiba endelevu kila siku.
“Inaweza kuwa ni muda wa chakula ama chai na muda mwingi ni kwa ajili ya mazoezi hilo ndilo ambalo tunafanya kila siku,” anamaliza Shaban.