CEO SIMBA,HAJI MANARA WAFUNGUKA BAADA YA KUITWA TFF

MTENDAJI Mkuu wa Klabu ya Simba Barbara Gonzalez na Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga Haji Manara leo wametinga katika Ofisi za Shirikisho la Mpira Tanzania, (TFF) ambapo waliiitwa kwa ajili ya kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya TFF.

Kila mmoja kwa nyakati tofauti kaweka wazi kwamba hakuna jambo ambalo wanaweza kuzungumza mpaka pale taarifa itakapotolewa.

Baada ya kutoka kuhojiwa na Kamati ya Maadili, CEO Barbara alisema hawezi kuongea chochote kwani wenye mamlaka ya kutoa tamko ni TFF.

Naye Haji Manara kwa upande wake amesema hawezi kuzungumza jambo lolote zaidi y kuawaachia wenye mamlaka kwa kuwa ni kesi.

“Hii ni kesi sasa mimi siwezi kuzungumza jambo lolote kuhusu hili na hakuna ugomvi sisi tulikuwa tunazungumza masuala yanayotuhusu,”.

Barbara aliandikiwa barua ya kufika katika Ofisi za TFF akiwa na tuhuma ya kufanya mahojiano na Chombo cha Habari cha nchini Afrika Kusini na kutamka baadhi ya maneno ambayo yanasemekana kuwa na ukakasi wa kuichafua Nchi, Klabu ya Yanga pamoja na Mpira wa Miguu wa Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake Haji Manara sababu ya wito wake imeelezwa kuwa ni maandishi ambayo alichapishwa kwenye mtandao wake wa kijamii kuhusu Simba.