KAZE:TUNAZITAKA POINTI TATU ZA MBEYA KWANZA

 CEDRICK Kaze, Kocha Msaidizi wa Yanga amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao wa ligi dhidi ya Mbeya Kwanza ambao unatarajiwa kuchezwa leo Mei 20, Uwanja wa Mkapa.

Yanga ni vinara wa ligi wakiwa na pointi zao 60 baada ya kucheza mechi 24 wanakibarua cha kusaka pointi tatu mbele ya Mbeya Kwanza ambao nao wanazihitaji pointi hizo.

Mbeya Kwanza imetoka kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Majimaji na Yanga imetoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri,Dodoma.

Kaze amesema wanajua mchezo huo utakuwa mgumu na watapambana kufanya vizuri ili kupata matokeo.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu hasa ukizingatia kwamba ni timu ambayo inahitaji pointi tatu na kila timu ni imara kwetu hivyo tunawaheshimu.

“Uzuri ni kwamba kila timu inafanya vizuri uwanjani hivyo ni muhimu kucheza kwa umakini kupata ushindi kwenye mchezo wetu,” amesema.

Mazoezi ya mwisho Yanga walifanya jana Mei 19 kwa ajili ya mchezo wa leo na miongoni mwa wachezaji ambao walifanya katika mazoezi hayo ni Fiston Mayele,Sure Boy na Khalid Aucho.