MJUMBE wa Kamati ya Mashindano ya Yanga na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, anajivunia usajili bora wa kiungo mchezeshaji, Salum Aboubakari ‘Sure Boy’ ambao umeongeza ubora wa kikosi chao.
Sure Boy ni kati ya wachezaji watano waliosajiliwa na Yanga katika dirisha dogo msimu huu akitokea Azam FC.
Wachezaji wengine waliosajiliwa na timu hiyo katika dirisha dogo ni Denis Nkane, Aboutwalib Mshery, Chico Ushindi na Chrispin Ngushi.
Hersi amesema usajili wa Sure Boy umejibu katika kikosi chao msimu huu na hilo tayari amelidhihirisha.
Hersi amesema kiungo huyo tayari amejihakikishia nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza, licha ya kukutana na ushindani mkubwa kutoka kwa viungo baadhi akiwemo Khalid Aucho, Yannick Bangala na Feisal Salum ‘Fei Toto’.
“Kama uongozi tuna kila sababu ya kujivunia usajili bora ambao tunaendelea kuufanya kila msimu.
“Dirisha dogo msimu huu, benchi la ufundi liliomba tufanye maboresho katika baadhi ya maeneo ikiwemo kipa, tukamleta Mshery ambaye anaonesha kiwango kikubwa.
“Pia benchi likaomba tusajili kiungo, basi tukamleta Sure Boy ambaye hivi sasa ni kati ya viungo tegemeo katika kikosi cha kwanza, kiungo huyo amethibitisha ubora katika timu kutokana na mchango anaoutoa, ninaamini ataifanyia makubwa zaidi Yanga siku za usoni,” amesema Hersi.