STRAIKA WA MABAO AKUBALI KUSAINI YANGA

BAADA ya tetesi nyingi kuzagaa kuhusishwa kusaini mkataba Yanga, mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole ametoa sharti moja kubwa kwa timu hiyo.

Mpole ni kati ya wachezaji wanaohusishwa kutua Yanga kuelekea msimu ujao ambapo timu hiyo ina uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mshambuliaji huyo hivi sasa yupo katika vita kubwa ya kuwania ufungaji bora ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu akifukuzana na straika wa Yanga, Mkongomani, Fiston Mayele. Kabla ya jana, wote walikuwa na mabao 12.

Akizungumza na Spoti Xtra, Mpole alisema timu zote zinazomuhitaji kwa ajili ya kuzungumza naye ili kumsajili, hivi sasa zimuache kwanza atimize majukumu yake katika kikosi cha Geita Gold.

Mpole alisema, hivi sasa akili yake ameiweka ndani ya Geita Gold kwa ajili ya kuipambania imalize ligi katika nafasi nzuri katika msimamo ambapo wanashika nafasi ya nne wakikusanya pointi 31.

“Zipo taarifa nyingi kunihusisha kuhitajika na baadhi ya timu za ligi kuu hapa nyumbani, lakini huu sio muda muafaka kwangu kuanza kufanya mazungumzo na timu yoyote.

“Kikubwa sitaki kuvuruga akili yangu, hivi sasa nguvu zangu nimezielekeza katika kuipambania timu yangu kwa michezo iliyobaki, lengo likiwa ni kumaliza tukiwa katika nafasi nne za juu.

“Hivyo hizo timu zinazonihitaji naomba ziniache kwanza hadi pale ligi itakapomalizika ndiyo tuanze kukaa meza moja kwa ajili ya kufanya mazungumzo.

“Hadi hivi sasa bado sijaamua hatma yangu wapi ninakwenda msimu ujao, nitatoa kipaumbele kwa timu yangu ya Geita Gold kabla ya kuchukua maamuzi mengine,” alisema Mpole.